Monday, 17 November 2014



KILIMO BORA CHA NYANYA
Utangulizi
Nyanya ni zao la chakula na biashara. Kilimo cha zao hili hufanyika majira yote (masika na kiangazi), na faida hupatikana haraka na ni ya kuridhisha ikilinganishwa na mazao mengine. Pamoja na umuhimu wa zao hili, wadudu waharibifu na magonjwa huathiri uzalishaji na ubora wa matunda. Ili mkulima aweze kupata faida na kuongeza pato la kaya yake ni vema kuzingatia udhibiti wa magonjwa na wadudu wa zao hili. Kipeperushi hiki kinatoa maelezo ya udhibiti wa magonjwa na wadudu muhimu ya zao la Nyanya.



MAGONJWA YA NYANYA
1.Bakajani chelewa (Late blight)
Ugonjwa huu huenenzwa na vimelea vya fangasi. Husababishwa na hali ya hewa hasa ya unyevunyevu, na huenezwa na upepo. Majani, shina, matunda hushambuliwa. Majani huwa na ukungu mweupe na kijivu, na baadaye hukauka. Matunda huwa na mabaka ya kikahawia na baadaye kuoza. Mashina pia huwa na mabaka ya kikahawia.
Udhibiti
· Nyunyiza dawa ya kuzuia ukungu hasa wakati wa masika, Dawa  inazopendekezwa ni Ridomil, Dithane 45, Bravo, Funguran, milraz. Fanya mzunguko wa mazao. Usipande nyanya sehemu moja kila msimu au palipolimwa mazao jamii ya nyanya km viazi mviringo, bilinganya, aina zote za pilipili na nyanya chungu.
· Tumia mbegu safi
· Panda aina za nyanya zinazovumilia ugomjwa

2.Bakajani tangulia (Early blight)
Huenezwa na vimelea vya fangasi. Husababishwa na kuenezwa na hali ya hewa pamoja na mbegu zenye ugonjwa. Mabaka ya kahawia yenye mistari ya mviringo huonekana kwenye majani na shina. Baka jeusi hutokea sehemu ya tunda inayoshikana na kikonyo.
Udhibiti
· Nyunyiza dawa ya Kocide, Funguran
· Teketeza mabaka ya mazao baada ya kuvuna
· Tumia mbegu safi na bora

3.Mnyauko fusari (Fusarium wilt)
Huenezwa na mbegu zenye ugonjwa. Husambazwa na vimelea vya fungasi vinavyoishi kwenye udongo. Ugonjwa hujitokeza zaidi wakati wa kiangazi. Vimelea hushambulia sehemu au mirija ya mmea ya kupitishia maji na chakula. Mmea hukosa maji na chakula na hatimaye hunyauka. Shina la mmea likipasuliwa ndani huonekana rangi ya kikahawia.
Udhibiti
· Tumia mbegu safi na bora
· Tumia mzunguko wa mazao. Nyanya zisizungushwe na mazao jamii yake
· Teketeza masalia ya mimea
· Choma kitalu cha nyanya kabla ya kusia mbegu

4.Mnyauko bacteria (Bacterial wilt)
Ugonjwa husababishwa na vimelea vya bacteria vinavyoishi kwenye udongo. Huenezwa na kusambazwa na mbegu na udongo wenye vimelea. Mirija ya mimea ya kupitishia maji na chakula hushambulia na mimea hunyauka ghafla. Mmea hukauka na kufa.
Udhibiti
· Panda mbegu safi
· Panda nyanya sehemu ambayo haijawahi kupandwa viazi mviringo, ilinganya au nyanya chungu
· Tumia mzunguko wa mazao
· Hakikisha mfereji wa maji ya kumwagilia hayapiti kwenye shamba lenye historia ya ugonjwa huu.
· Choma kitalu cha nyanya kabla ya kusia mbegu

5. Mnyauko vetisili (Verticillum wilt)
Hakuna dawa inayozuia au kutibu ugonjwa huu kwa sasa. Ugonjwa husababishwa na ukungu (fangasi) kwenye udongo. Ukungu huu huishi kwenye udongo kwa muda mrefu bila kudhurika. Ugonjwa huongezeka ikiwa mizimizi ya nyanya imeshambuliwa na minyo fundo; au kukiwepo na hali ya ubaridi au ukame. Ugonjwa husababisha hasara kubwa. Ugonjwa hushambulia sehemu ya ndani ya shina na
kusababisha sehemu hiyo kuwa na rangi ya kijivu. Majani hugeuka njano na mimea kunyauka na kufa.
Udhibiti
· Tumia mzunguko wa mazao usiopungua miaka mine
· Ondoa mabaki ya nyanya shambani
· Tumia mbegu bora na safi

6. Bakadoa (Bacterial spot)
Ugonjwa huu huenezwa na vimelea vya bacteria vinavyoishi kwenye mbegu, pia kwenye hewa. Huenezwa kwa kasi sana wakati wa masika. Madoa ya rangi kahawia huonekana kwenye majani na matunda.
Udhibiti
· Panda mbegu bora na safi
· Tumia mzunguko wa mazao
· Teketeza masalia ya mazao
· Nyunyizia dawa ya funguran, Kocide101, Cobox, Bravo

7. Makovu bakteria (Bacterial canker)
Ugonjwa huenezwa na vimelea vya bacteria vinavyoishi kwenye mbegu na hewani. Hutokea zaidi wakati wa masika. Majani hukauka nchani na makovu yaliyodidimia hutokea kwenye shina. Matunda huwa na makovu yenye rangi ya kahawia sehemu ya katikati.
Udhibiti
· Tumia mbegu bora na safi
· Teketeza masalia ya mazao
· Tumia mzunguko wa mazao

8. Rasta (Yellow leaf curl)
Ugonjwa huu husababishwa na virusi na huenezwa na nzi wadogo weupe. Hutokea zaidi wakati wa kiangazi. Mimea hudumaa na majani yaliyoshambuliwa huwa na rangi ya manjano na pengine rangi ya zambarau. Nyanya hupasuka.
Udhibiti
· Nyunyiza dawa za sumu za kuua wadudu (Selecron, Dursburn, Actelic)
· Ng’oa mimea yenye ugonjwa
· Tumia mzunguko wa mazao
· Weka shamba katika hali ya usafi

9. Batobato (Tomato mosaic virus)
Ugonjwa husababishwa na virusi na hueezwa na mbegu na kugusana. Majani huwa na mchanganyiko wa rangi hasa kijani kibichi na kijani kilichofifia (majano). Majani hujikunja na manjani machanga huwa na maumbile yasiyo kawaida. Ukifikisha jani huwa linavinjikavunjika.
Udhibiti
· Tumia mbegu bora na safi
· Ng’oa mimea iliyoshambuliwa
· Teketeza masalia ya mazao
· Weka shamba katika hali ya usafi

WADUDU WAHARIBIFU
1.     Viwavi Matunda (Fruit worm)
Viwavi hawa hutokana na wadudu nondo. Viwavi hutoboa matunda na kuacha matundu na hatimaye matunda huoza. Hupunguza ubora wa matunda.
Udhibiti
Nyunyizia dawa ya kuua wadudu. Dawa hizo ni pamoja na Actelic 50EC, Selectron, Dursbaan, Maji ya majani ya mwarobaini au utupa pia huua wadudu.

2.     Utitiri wekundu (Red Spider mites)
Hawa ni wadudu wekundu, wadogo sana wanaoweka utando chini ya majani, hasa wakati wa kiangazi. Wadudu hawa hufyonza utomvu kwenye majani na kusababisha majani kukauka.
Udhibiti
· Nyunyizia dawa za sumu. Dawa hizo ni pamoja na Actellic, Selecron, Dursbarn na Thionex
· Mwagilia maji mara kwa mara
· Weka shamba katika hali ya usafi

3.     Inzi weupe (White flies)
Hawa ni Inzi weupe wadogo sana. Hujitokeza sana wakati wa kiangazi. Hueneza ugonjwa wa virusi ujulikanao kama Rasta.
Udhibiti
Nyunyizia dawa za sumu za kuulia wadudu kama Selecron, Actellic, Dursban na thionex. Pia maji ya majani ya mwarobaini na utupa.

4.     Vidukari au Wadudu mafuta (Aphids)
Ni wadudu wenye rangi nyeusi au kuijani au kahawia. Hukaa chini ya majani na kufyonza utomvu kwenye majani machanga. Hudumaza mmea na kushindwa kuzaa matunda
Udhibiti
Nyunyizia dawa za sumu za kuulia wadudu kama Rogor, Actellic, Selecron, Dursban, maji ya majani ya mwarobaini na utupa, maji ya pilipili.

5.     Minyoo (Nematodes)
Ni minyoo midogomidogo ambayo hushambulia mizizi na kuweka vifundo. Mizizi hushindwa kuchukua maji na chakula kwenye udongo. Mimea hudumaa na kushindwa kuzaa
Udhibiti
· Tumia mzunguko wa mazao
· Choma udongo wa kitalu kabla ya kusia mbegu kwa kutumia karatasi la plastiki jeusi na nishati ya jua
· Choma masalia ya mazao

6.     Sota (Cutworms)
Hushambulia miche ya nyanya hasa baada ya kupandikizwa shambani. Wakati wa mchana hujificha kwenye udongo na usiku hujitokeza na kukata miche kwenye shina usawa wa udongo.
Udhibiti
· Nyunyiza dawa za kuua wadudu kwenye shina usawa wa udongo
· Hakikisha miche inapata maji ya kutosha.

No comments:

Post a Comment